Panga Vilivyo Kipaumbele
We're glad you like it!
Enjoying the content? You can save this to your favorites by logging in to your account.
Matendo 20:24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.
Je! Ni mara ngapi unavyotafakari vilivyo kipaumbele? Ni mara ngapi unapima mambo kichwani na moyoni pia ili yakusaidie kuamua kilicho muhimu zaidi? Je! Inanipasa nifanye nini leo na kesho na kesho kutwa?
Watu wengi hawachukui nafasi hata kidogo kutafakari swala la kipaumbele katika maisha kwa sababu wako bizi sana kwa kukumbana na matukio ya maisha haya, wakipambana na milima na mabonde na jinsi hisia zao zinavyopanda na kushuka. Wengine wanasumbuliwa mno, wakijitahidi wasimezwe kabisa na hali ngumu. Sijui kama umeshaona hayo?
Katika hali kama hiyo, kinachotawala mawazo yetu kwanza kabisa ni usalama wetu na jinsi tunavyoweza kunusurika katika shida. Pili, tunataka starehe. Sote tunataka kuwa salama na kuwa na starehe. Kwa hiyo, bila hata kufikiria, hii ndiyo njia tunapitia karibia kila mara, si kweli?
Halafu maisha yakitupiga chenga, mambo yakienda kombo kabisa, tunashtuka na kuchukia na kujaribu kwa njia zote kujilinda na kuepukana na madhara. Lakini sivyo alivyofanya Mtume Paulo. Yeye alikuwa amejiwekea taratibu tofauti kabisa kuhusu kilicho kipaumbele:
Matendo 20:22,23 Basi sasa angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.
Na kweli, ndivyo ilivyomtokea wakati alifika Yerusalemu. Sasa, ni kipi kilichomsukuma aendelee kuelekea kule? Aliwezaje kufuata njia hiyo?
Matendo 20:24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.
Rafiki yangu, panga sawa sawa vilivyo kiapumbele katika maisha yako.
Hili ndilo Neno la Mungu safi na lenye afya kwa ajili yako leo.